BODI YA WAKURUGENZI YA NEMC YAFANYA ZIARA KATIKA MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE


Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), wakiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza pamoja na Wataalamu wengine, wamefanya ziara katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere uliopo katika Bonde la Mto Rufiji ambao bado upo katika hatua za ujenzi ili kujionea hali halisi ya kimazingira katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo. Mradi unategemewa kuzalisha MW 2115 za umeme ifikapo mwaka 2022. Pamoja nakuzalisha umeme mradi huu pia utasaidia kudhibiti mafuriko na kutunza mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Muhandisi Prof. Esnat Chagu ameeleza kuwa Bodi imeamua kutembelea mradi huu ili kujionea namna ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi unavyozingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kuepusha athari mbalimbali za kimazingira zitakazo weza kujitokeza.

“Mradi huu ni mkubwa sana ambao una faida nyingi sana kwa nchi yetu,pamoja na hivyo tunahitaji kuzingatia na kuhakikisha ujenzi huu unafanyika bila kuathiri mazingira yetu kwa kiasi kikubwa.” alisema Muhandisi Prof. Chagu.

Aliendelea kusema kuwa anaunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kujitoa kutekeleza mradi huu kwani unafaida kubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu na utasaidia kutekeleza azimio ya kauli mbiu ya awamu ya tano ya “Tanzania ya Viwanda” kwani umeme mwingi utapatikana na kupelekea ukuaji wa viwanda nchini na uwekezaji kwa ujumla. Pamoja na kuzalisha umeme, utakapo kamilika mradi huu patakuwa na sehemu ya kivutio cha utalii na utawavutia wawekezaji wengi na itapelekea kuongeza idadi ya wawekezaji Nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la hifadhi na usimamizi wa Mazingira Muhandisi Dkt. Samuel Gwamaka ameeleza kuwa “Tumekagua maeneo ya Mradi na kujionea hali halisi ya kimazingira na tumeona yanaridhisha sana. Lakini pia nichukue fursa hii kumpongeza Mhe. Rais pamoja na serikali yake kwa juhudi waliyoionesha kupambania uwekezaji wa mradi huu mkubwa ambao utakuwa na faida kubwa kwa kizazi kilichopo na kijacho, hivyo niwaombe wananchi kuunga mkono juhudi hizi ili kutimiza azimio hilo”

Aidha, Mkuu wa Idara ya Afya, Usalama na Mazingira wa mradi, Muhandisi Dkt. Mabula Majige, ameeleza kuwa amefurahishwa na ujio wa Bodi ya NEMC kwani wao ni wadau wakubwa sana wa usimamizi na uhifadhi wa mazingira nchini. Kutokana na mradi huu kufanyika katika mazingira ambayo ni nyeti hivyo ujio wao umekuwa ni wa muhimu sana. Shughuli za ujenzi wa mradi huu unazingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

“Mpaka sasa hivi mradi upo katika mazingira mazuri yanayoridhisha tumejitahidi kuzuia uchafuzi, kudhibiti mitetemo ili kuepusha usumbufu kwa wanyama, kuepusha athari za mafuriko kwa wakazi wanaokaa karibu na mradi, na kwa upande wa usalama wasimamizi wa mradi wanajitahidi kusimamia na kusisitiza wafanyakazi wa mradi kutii sheria za kazi kuvaa vifaa vya kinga ili kuepusha ajali zisizo za lazima. Kwa maana hiyo afya, usalama kazini na hali ya mazingira vinaendelea vizuri katika mradi huu.”

Naye Msaidizi wa Idara ya Afya, Usalama na Mazingira wa mradi, Muhandisi Bahati Buzenganwa, ameleza kuwa utekelezaji wa mradi huu umezingatia utunzaji wa mazingira kwani wamefanikiwa kuweka miundo mbinu inayoweza kudhibiti taka ngumu na maji taka yanayozalishwa na wafanyakazi.

“tumejitahidi kusimamia utunzaji wa mazingira kwani usalama wa maisha yetu yanategemea mazingira yalio bora na salama hivyo kwa upande wa mradi huu tumejitahidi kuzingatia hilo. Kumekuwa na desturi ambayo ya kutenganisha taka baada ya kuzalishwa kabla ya kukusanywa kwa ajili ya kwenda kutupwa. Huu ni utaratibu unaotekelezwa kutokana na baadhi ya maelekezo yaliyotolewa na NEMC baada ya kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira ya mradi huu”

Ujumbe huo kutoka NEMC ulifarijika kuona utaalamu mkubwa unafanyika kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo hauthiri Mazingira. Ujumbe huo pia ulipata fursa ya kutoa ushauri mbalimbali wa jinsi ya kuyaboresha zaidi mazingira kwa ujumla.

Mradi wa Umeme wa Julias Nyerere ambao uta gharimu takriban Shillingi Trillion 6.6 pindi utakapo malizika, umepangwa kufanyika ndani ya miezi arobaini na mbili (42) ambayo maandalizi ya mradi ni miezi sita(6) na ujenzi wa mradi ni miezi thelathini na sita (36). Ujenzi wa mradi umeanza tarehe 15 Disemba 2018 na unatarajiwa kukamilika tarehe 14 juni 2022.

Faidaza mradi huu zimeanza kuonekana kuanzia hatua za ujenzi kwani rasilimali za ujenzi zinatoka nchini kwa kiasi kikubwa na asilimia 90% ya wafanyakazikatika sekta za mbali mbali za mradi huo ni Wazawa. Pia faida zitakazo patikana baada ya kukamilika kwa mradi huu ni kubwa sana katika nchi yetu kwani utasaidia kupatikana kwa umeme wa kutosha utakaotumika majumbani, na katika sekta mbalimbali ikiwema ya uwekezaji. Pia itasaidia kupatikana kwa umeme wa bei nafuu na kupelekea kupunguza matumizi ya nishati nyingine ambazo sio rafiki kwa mazingira yetu.