KAMATI YA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA ZANZIBAR YAZURU NEMC
Kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa Zanzibar imetembelea ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa masuala ya Mazingira.
Kamati hiyo iliyoambatana na timu ya watu 31 imepata fursa ya kutembelea mradi wa treni ya umeme ya SGR Kituo Kikuu cha Dar es salaam ili kupata taarifa sahihi za jinsi mradi huo unavyozingatia masuala ya utunzaji wa Mazingira.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu Zanzibar Mhe. Machano Othman Said amelipongeza Baraza kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia Mazingira kwenye miradi mikubwa ya kimkakati na ya maendeleo kama mradi wa treni ya umeme SGR Nchini Tanzania.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NEMC Mhandisi Prof. Esnati Chaggu amesema Baraza linazingatia Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kanuni zake na kuhakikisha elimu juu ya Mazingira inatolewa kwa jamii.
“Jukumu la Baraza ni kuhakikisha Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Mazingira unazingatiwa. Baraza limelenga kuwafikia wananchi na kuwapa elimu ya utunzaji wa mazingira kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, Hivyo Baraza linaendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa juu ya masuala ya mazingira “ amesema Mhandisi Prof. Esnati Chaggu.
Kadhalika Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii NEMC Bi. Lilian Lukambuzi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu NEMC ameeleza juhudi za Baraza hasa katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki inavyorahisisha utekelezaji wa majukumu ya Baraza hali iliyorahisisha huduma kwa wadau wa Mazingira Nchini.
Akiwasilisha wasifu wa Baraza la Mazingira Dkt.Rose Salema amesema Baraza katika utekelezaji wa majukumu yake linasimamia misingi ya Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake.
Katika ziara hiyo iliyokuwa na timu ya watu 31 imehusisha watumishi kutoka Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar na Mamlaka ya Mazingira Zanzibar (ZEMA) ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Shekha Mjaja Juma.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15