NEMC YATOZA FAINI KIASI CHA BILIONI 5.1 KAMPUNI ZA MAFUTA.


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka kwa mamlaka aliyopewa amevitoza faini vituo vya mafuta vinavyomilikiwa na Makampuni mbalimbali ya uuzaji na usambazaji wa Mafuta Nchini jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 5.1 kwa kushindwa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM). Ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Akiongea katika Mkutano huo ametaja Kampuni pamoja na idadi ya vituo na faini waliyotozwa kuwa ni pamoja na Oryx Tanzania L.t.d vituo kumi na tano na faini ya shilingi milioni 750, Kampuni ya PUMA vituo ishirini na mbili na faini ya shilingi bilioni 1.1, Kampuni ya TOTAL vituo kumi na sita na faini ya shilingi milioni 800, Kampuni ya Camel vituo sita na faini ya shilingi milioni 300, Kampuni ya GBP vituo kumi na faini ya shilingi milioni 500, Kampuni ya GAPCO vituo nane na faini ya shilingi milioni 400, Kampuni ya Esta vituo tisa na faini ya shilingi milioni 450, Kampuni ya Oilcom vituo kumi na mbili na faini ya shilingi milioni 600 na Kampuni ya TSN Vituo vinne na faini ya shilingi milioni 200.

Amemaliza kwa kusema kuwa mpaka sasa Kampuni za uuzaji na usambazaji wa mafuta zilizotozwa faini ni Kampuni 10 na tayari wameshatoza faini ya kiasi cha shilingi bilioni 3.3 Kampuni ya Lake Oil.

'‘Mpaka sasa Kampuni zilizotozwa faini ni Kampuni kumi na NEMC bado tunaendelea na msako kwa Makampuni yote ambayo hayajafanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na ninawaomba wajisalimishe”.amesema Dkt. Gwamaka