NEMC YAWASILISHA TAARIFA YA MRADI WA KUPUNGUZA MATUMIZI YA ZEBAKI KWA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa kupunguza matumizi ya Zebaki kwa Kamati za Kudumu za Bunge ambazo ni Kamati ya Biashara, Viwanda na Mazingira na Kamati ya Nishati na Madini katika Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.

Taarifa hiyo inalenga kujenga uwezo na uelewa kwa wabunge kuhusu mradi huona utekelezaji unaofanyika katika kupunguza na ikibidi kuondoa kabisa matumizi ya Zebaki nchini. Kama inavyo fahamika matumizi ya Zebaki katika shughuli za uchenjuaji wa dhahabu yana madhara makubwa katika mazingira, viumbe hai na hasa afya ya binadamu.

Aidha muwasilishaji wa taarifa hiyo kutoka NEMC Muhandisi Benjamin Mchwampaka amesema kuwa, imebainika utumiaji wa Zebaki katika uchenjuaji dhahabu unaofanywa na wachimbaji wadogo una madhara makubwa, ikiwemo kuathirika kwa mfumo wa fahamu, kuharibika kwa mimba, kuzaa wenye vichwa vikubwa, kuharibika kwa figo, ngozi na kulegea kwa misuli. Hizi ni miongoni mwa athari zinazotokana na matumizi ya Zebaki hivyo ndio maana Serikali kupitia mradi huu ina mpango wa kupunguza na ikiwezekana kuyatokomeza kabisa matumizi ya katika shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu. Mradi huu unajikita hasa katika utoaji elimu kwa wadau wa ngazi zote na kutafuta njia mbadala zisizohusisha zebaki katika echenjuaji dhahabu ambazo wachimbaji wadogo wataweza kuzitumia.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa mradi wa kudhibiti athari za Zebaki unalengo la kupunguza au kutokomeza kabisa matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo, hivyo kuna haja ya kushikamana kama serikali kutokomeza kabisa suala hili

"Jambo hili ni kubwa sana na linataka nguvu ya pamoja katika kulitekeleza hivyo tunahitajimichango ya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo Wizara na Sekta zote husika ili kufanya janga hili lisije kuwa kubwa zaidi huko mbeleni"

Pia Mhe.Jafo amewataka wataalamu wake kupokea maoni kutoka kwa wadau na kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya athari ya matumizi ya Zebaki. Amesema sehemu zinazopatikana dhahabu nchinikama kanda ya Ziwa na kwingineko ndio watumiaji wakubwa wa Zebaki hivyo kuna haja ya kutafuta mbinu mbadala iliyobora ya kutumia huku tukiendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya athari ya kutumia Zebaki katika shughuli zao za uchenjuaji dhahabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt.Samuel Gwamaka, amesema kuwa sehemu kubwa ya fedha za Mradi huu ni kuwawezesha wanasayansi kufanya tafiti kuona ni mbinu gani mbadala inayoweza kutumika na wachimbaji wadogo kwani wao ndio wanaoathirika sana na ndio watumiaji wakubwa wa Zebaki katika kufanya shughuli zao.

Vile vile katika mkutano huo Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira kutoka NEMC, Dkt. Menan Jangu, alitoa elimu kwa Kamati hizo za Kudumu za Bunge juu ya umuhimu wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) ili kufikia maendelea yasiyoathiri mazingira kwa kiwango kikubwa. Dkt. Menan amesema kwa kuwa Nchi imejikita katika kukuza uchumi wa viwanda na kuboresha maisha ya wananchi, changamoto za kimazingira haziepukiki, hivyo ili kuweza kuepusha changamoto hizo kuna haja ya kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa kila Mradi wa maendeleo unaotaka kuanzishwa Nchini.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe.Seif Khamis Gulamali, amemalizia kwa kusema kuwa kutokana na hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge baada ya kuwasilisha taarifa ya Mradi wa kudhibiti matumizi ya zebaki ni vizuri kuenda katika maeneo hayo ambayo shughuli za uchimbaji zinafanyika ili kuweza kujionea hali halisi ya jamii ya watu wa huko.