VIWANDA ACHENI KUTIRIRISHA MAJI MACHAFU- WAZIRI UMMY MWALIMU


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu amevitaka viwanda vyote Nchini kuacha mara moja kutiririsha maji taka yasiyotakaswa kutoka katika viwanda vyao kwani ni uharibifu wa mazingira.

Ameyasema hayo mjini Kibaha alipokua kwenye ziara ya Mkoa wa Pwani kuangalia hali ya kimazingira katika mkoa huo ambapo alitembelea kiwanda cha kuchakata shaba cha Futan Mining International Ltd na kiwanda cha sabuni na misumari cha Prance International Trading Ltd kwa ajili ya kukagua masuala ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Akiongea katika kiwanda cha Prance kilichopo Misugusugu mjini Kibaha, Waziri Ummy amekipongeza kwa kutumia nishati ya makaa ya mawe badala ya kuni kama viwanda vingine. “Nawapongeza sana kwa kutotumia kuni kama nishati na kwa kuwa inapelekea uharibifu mkubwa wa mazingira, pia nawapongeza kwa kuwa na mtambo wa kutakasa maji taka kutoka kiwandani, naagiza na viwanda vingine vyote viige mfano huu”,alisema Waziri Ummy.

Aidha akiwa katika kiwanda cha Futan Waziri Ummy alitaka kiwanda hicho kuutoa mara moja mfumo wa kutakasa majitaka waliouweka katika bonde la mto lililo kando ya kiwanda hicho kwani wanakiuka sheria ya mazingira na kupelekea kuharibu na kuchafua mfumo wa maji wa mji wa Kibaha na kuhatarisha afya ya wanaotumia maji hayo. "Muondoe mara moja mfumo wa utakasaji maji taka kutoka katika bonde hili" alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy pia alisema kuwa ingawa viwanda ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi lakini lazima kuwe na uwiano mzuri kati ya uwekezaji na utunzaji wa Mazingira.

Pia alisema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na NEMC, itaendelea kusaidia wenye viwanda ili kuhakikisha uwekezaji unafanyika bila kuathiri mazingira.

Waziri Ummy pia alitembelea Dampo la Kibaha ambapo aliagiza Halmashauri iweke miundombinu mizuri ya usimamizi wa taka kwa kujenga vizimba na Dampo la kisasa na kuhakikisha taka zinatengenishwa kuanzia ngazi ya kaya ili kupunguza gharama za usafirishaji wa taka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Mhe. Evarist Ndikilo akimkaribisha Waziri Ummy alisema kuwa Mkoa wa Pwani una changamoto kubwa ya biashara ya uchimbaji wa mchanga ambapo biashara hiyo inasababisha mashimo makubwa ambayo ni uharibifu wa mazingira na kusababisha mashimo hayo kujaa maji wakati wa mvua. "Biashara ya uchimbaji wa mchanga katika mkoa wa Pwani ni biashara ambayo inaharibu sana mazingira" alisema Mhandisi Ndikilo.

Waziri Ummy yuko katika ziara ya siku 3 katika Mkoa wa Pwani kwa kutemblea mkoa huo kujionea changamoto mbalimbali za utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika mkoa huo.