WAZIRI JAFO AFUNGUA KIKAO KAZI KWA MAAFISA MAZINGIRA NCHI NZIMA JIJINI DODOMA.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amefungua kikao kazi cha Maafisa mazingira nchi nzima kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao kazi hicho kimejuisha Maafisa mazingira nchi nzima kutoka Mikoa na Halmashauri zote nchini, wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na bodi ya wakurugenzi kutoka NEMC na wadau mbalimbali wa mazingira kutoka nchi nzima.

Akiongea kwenye kikao kazi cha Maafisa wa mazingira Mhe. Jafo amesema Maafisa mazingira ni watu muhimu sana katika ustawi wa mazingira yetu kwasababu ndiyo watekelezaji wa sera na sheria za mazingira katika maeneo yetu, hivyo kukutana nao ni moja kati ya njia pekee ya kujua nini changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa sheria za mazingira na kutatua changamoto hizo.

Mhe. Jafo ameongeza kuwa ni faraja kubwa sana kukutana na Maafisa mazingira nchi nzima, lengo kubwa ni kubadilishana mawazo na kupanga mipango mkakati ambayo itawezesha utekelezaji wa kanuni, sera na sheriayetu ya mazingira ili Nchi yetu isonge mbele kwenye suala zima la utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Hali kadhalika Mhe. Jafo amezungumzia kuhusu kaulimbinu ya Siku ya Mazingira Duniani Kitaifa ambayo ni “TUTUMIE NISHATI MBADALA KUONGOA MFUMO IKOLOJIA” kwamba dunia ipo kwenye hatari ya mabadiliko ya tabianchi. Mabadiliko haya yanasabaishwa na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kama ukataji wa miti, na uchomaji wa mkaa. Athari zinazojitokeza kutokana na uharibifu huo ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha maji kwenye bahari na maziwa.

Mhe. Jafo amegusia pia suala la uchafu katika mazingira yetu kuwa ni suala ambalo linahitaji kuchukuliwa hatua za haraka, mfano kuna baadhi ya madampo ambayo hayatumiki ni lazima sasa yaangaliwe namna ya kuyatumia ili kuondoa uchafu katika mazingira yetu.Maafisa mazingira kwenye Serikaliza mitaa wamepewa jukumu la kusimamia mazingira katika maeneo ya mitaa, hivyo amewaomba wakafanye kazi kikamilifu ili kulinda na kuhifadhi mazingira yetu.

Naye Naibu Waziri wa Ofisi ya RaisTAMISEMI Dkt. Festo Dugange amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI kutokana na maelekezo ya mgawanyo wa majukumu uliotolewa na Mhe. Rais inatekeleza majukumu ya kiutendaji, usimamizi na kuratibu utekelezaji sera na mipango ya kisekta katika ngazi ya Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa. Dkt. Dungage ametoa maelekezo kwa Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa kuwa suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira liwe ni jambo la kila siku. Ni lazima zisimamie sera na sheria za mazingira ili nchi yetu iwe sehemu safi na salama.

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya NEMC Prof. Esnath Chaggu ameongeza kuwa Siku ya Mazingira Duniani inatukumbusha wajibu wa kutunza mazingira kwa faida ya kizazi hiki na kijacho. Kikao kazi hiki kitasaidia kutoa mambo yenye tija kuhusu mazingira yetu kwasababu tunaojadili ndiyo watekelezaji wa sera za mazingira.