WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) MHE. UMMY MWALIMU AWASILI KATIKA OFISI ZA BARAZA LA TAIFA LA HIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA (NEMC) BAADA YA UTEUZI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Ummy Mwalimu , amesema kuwa ongezeko la joto, uchafuzi wa hewa, ni kati ya changamoto zinazotokana na uharibifu wa mazingira ambao unatokana na ukataji miti hovyo na ongezeko la shughuli za kijamii na kiuchumi ambazo zinafanywa na wananchi bila kujali utunzaji wa Mazingira.

Aliyasema hayo leo hii alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya NEMC na waandishi wa habari baada ya kupokelewa katika ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mikochenijijini Dar es Salaam, baada ya kuapishwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Desemba 9, 2020 jijini Dodoma.

“Tumekubaliana na NEMC kuwa tutaendelea kutoa elimu kwa Wananchi kutambua umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazigira na kwenye hili tumebainisha maeneo makubwa manne ambayo tutayafanyia kazi ili kutunza mazingira. Maeneo hayo ni Viwanda, Migodi, Ujenzi holela katika vyanzo vya maji, pamoja na vyuma chakavu”

Ameendelea kusema kuwa kuna changamoto pia katika ucheleweshwaji wa kutolewa kwa vyeti vya Mazingira, kwani kumekuwa na malalamiko mengi yanayotolewa na wawekezaji ndani ya Nchi na kusababisha ucheleweshwaji wa maendeleo katika Nchi yetu

“Katika hili tumekubaliana na NEMC kuharakisha mchakato wa kutoa vibali vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na kuhakikisha vibali hivyo vinatolewa kwa wakati. Hata hivyo nimebaini kwamba ucheleweshwaji wa vibali hivyo kwa kiasi kikubwa hausababishwi na NEMC bali changamoto kubwa iko kwa wale washauri elekezi ambao ndio wanafanya hizo Tathmini za Athari kwa Mazingira. Hivyo kuna haja kubwa kuwasimamia washauri elekezi wa mazingira ambao sio waaminifu. Katika kusimamia hilo tutahakikisha tunaunda kanuni mpya ambazo zitasimamia wataalamu hao”

Ameendelea kusema kuwa katika maswala ya vyuma chakavu pia imekuwa ni changamoto kubwa hivyo kuna haja ya kutoa elimu kwa umma ili kutambua taratibu na mambo ya kuzigatia katika utoaji vibali vinavyotolewa kwa wakusanyaji, wahifadhi, na wasafirishaji wa vyuma chakavu.

“Katika hili kuna haja ya usimamizi ulio wa hali ya juu kwani hata Mhe. Rais alilieleza wakati ananiapisha hivyo tutalisimamia kikamilifu ili kufikia azma ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Kama mnavyo fahamu ukusanyaji wa vyuma chakavu pia ni sehemu ya kuondoa taka zilizopo katika maeneo yetu, lakini hatutaki biashara hio ikahujumu miundombinu ya Serikali kwa hiyo tutakuwa makini zaidi kuhakikisha vile vyuma chakavu ni kweli vyuma chakavu na havijang’olewa kutoka kwenye mataruma ya reli au madaraja”

Mhe. Ummy Mwalimu amemalizia kwa kusema kuwa kutokana na NEMC kuwa na Ofisi za Kanda Nchi nzima hivyo amewataka watumie zaidi ofisi hizo kuliko kazi nyingi kufanyika Makao Makuu. Hivyo ameagiza wataalamu waongezwe katika ofisi hizo ili kurahisisha utendaji wa kazi na kuweza kwenda na kasi ya Mhe. Rais.